Jeremiah 16

Siku Ya Maafa

1Kisha neno la Bwana likanijia: 2 a“Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.” 3 bKwa maana hili ndilo asemalo Bwana kuhusu wana na binti wazaliwao katika nchi hii, na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao, na wale wanaume ambao ni baba zao: 4 c“Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyosambaa juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa, nazo maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.”

5Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga, usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeziondoa baraka zangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asema Bwana. 6 d“Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, na hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao. 7 eHakuna yeyote atakayewapa chakula ili kuwafariji wale waombolezao kwa ajili ya wale waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, wala hakuna yeyote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji.

8 f“Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu, na kuketi humo ili kula na kunywa. 9 gKwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako, nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, na pia sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’

10 h“Utakapowaambia watu hawa mambo haya yote na wakakuuliza, ‘Kwa nini Bwana ameamuru maafa makubwa kama haya dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi ya Bwana, Mungu wetu?’ 11 iBasi waambie, ‘Ni kwa sababu baba zenu waliniacha mimi, wakafuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Waliniacha mimi na hawakuishika sheria yangu,’ asema Bwana. 12 j‘Lakini ninyi mmetenda uovu zaidi kuliko baba zenu. Tazama jinsi ambavyo kila mmoja wenu anafuata ukaidi wa moyo wake mbaya, badala ya kunitii mimi. 13 kKwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwatupa katika nchi ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua, nako huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, kwa maana sitawapa fadhili zangu huko.’

14 l“Hata hivyo, siku zinakuja,” asema Bwana, “wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’ 15 mbali watasema, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewatoa wana wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia.’ Maana nitawarudisha katika nchi niliyowapa baba zao.

16 n“Lakini sasa nitawaagiza wavuvi wengi,” asema Bwana, “nao watawavua. Baada ya hilo, nitawaagizia wawindaji wengi, nao watawawinda kwenye kila mlima na kilima, na katika nyufa za miamba. 17 oMacho yangu yanaziona njia zao zote, hazikufichika kwangu, wala dhambi yao haikusitirika. 18 pNitawalipiza maradufu kwa ajili ya uovu wao na dhambi yao, kwa sababu wameinajisi nchi yangu kwa maumbo yasiyo na uhai ya vinyago vyao vibaya, na kuujaza urithi wangu na sanamu za kuchukiza.”
19 qEe Bwana, nguvu zangu na ngome yangu,
kimbilio langu wakati wa taabu,
kwako mataifa yatakujia
kutoka miisho ya dunia na kusema,
“Baba zetu hawakuwa na chochote zaidi ya miungu ya uongo,
sanamu zisizofaa kitu
ambazo hazikuwafaidia lolote.

20 rJe, watu hujitengenezea miungu yao wenyewe?
Naam, lakini hao si miungu!”


21 s“Kwa hiyo nitawafundisha:
wakati huu nitawafundisha
nguvu zangu na uwezo wangu.
Ndipo watakapojua
kuwa Jina langu ndimi Bwana.
Copyright information for SwhKC